NEWS - MPYA ABOUT XPLASTAZ / KUHUSU KIKUNDI MAASAI LISTEN/SIKILIZA LINKS / VIUNGO GUESTBOOK / KITABU CHA WAGENI CONTACT / WASILIANA GALLERY MEMBERS - WALIOMO HISTORY (ENGLISH) FACTS AGENDA / RATIBA RELEASES  YAMAT OLE MEIBUKO - MEREGE

Yamati Ole Meibuko amezaliwa katika kijiji kijulikanacho kwa jina la "ELUWAI" kilichopo mkoani Arusha Wilaya ya Monduli nchini Tanzania Afrika ya mashariki. Kabila lake ni Maasai.

Rika
Kwa kawaida katika kabila la kimaasai kuna rika mbalimbali kutokana na Jando. Rika hufungwa na kufunguliwa kila baada ya miaka saba. Rika lake Merege ni "KORIANGA" Rika hili lilifunguliwa mwaka 1997 na litafungwa mwaka 2003.

Katika picha (kushoto): Yamat akichoma nyama ya mbuzi kwenye olpuri kwao Monduli, wakati wa kutengeneza video mpya ya X Plastaz (Mai 2002)



Familia
Yamat ni mtoto wa kwanza katika familia yao na baba yake ana wake wawili na mama yake Yamat ni mke mdogo yaani mke wa pili. Kwa kawaida katika jamii ya kimasai huwa wana uwezo wa kufunga ndoa na wanawake wengi iwezekanavyo kutokana na uwezo wa mwanamme. Kwa upande wa mama yake Yamat ana watoto watano na upande wa mke mwingine ana watoto sita, kwa ujumla baba yake ana watoto kumi na moja na kati yao wote Yamat ndie kaka yao mkubwa.

Kazi anazofanya kwa ujumla
Kwa kawaida kazi kubwa ya jamii ya Maasai ni ufugaji na kwa maana hiyo Merege ni mfugaji. Ambapo alianza shughuli ya ufugaji akiwa na umri mdogo kabla ya kutahiriwa yaani kabla ya kuwa Morani [Warrior].
Na katika umri huo Merege aliutumia muda huu katika kujifunza mbinu mbalimbali za kujikinga na kujilinda dhidi ya maadui na pia kujifunza mambo mbalimbali yanayohusiana na tamaduni, mila na desturi zao kama vile madawa n.k.

Shule
Yamat hakubahatika kwenda shule katika umri muafaka na hakuna hata mmoja katika familia yake aliyebahatika kusoma. Katika jamii ya Maasai huwa hawapendi kuwaruhusu watoto wao kwenda shule kwa kuhofia kupoteza mila na desturi zao na kuiga tabia za makabila mengine yaishiyo mjini.
Kwa sasa ameanza kujifunza kiingereza na lugha zingine mbalimbali ili kuweza kuwasiliana na makabila mbalimbali kitaifa na kimataifa. Kwa kipindi hiki anapokuwa mjini kwa shughuli ya masomo, huwaachia wadogo zake mamlaka ya kulisha na kuilinda mifugo yake pamoja na baba na mama. Kila mwisho wa wiki anakwenda kijijini kusalimia ndugu, jamaa, marafiki pamoja na kuangalia maendeleo ya mifugo na shamba lake kwa ujumla.

Muziki
Nadhani wote tunatambua nini maana ya muziki.

Muziki ni sehemu mojawapo ya maisha katika jamii ya wamaasai. Wamaasai wana imani ya kwamba kucheza na kuimba ni sawa na dawa. Muziki ni chombo au silaha wanayoitegemea katika kufikisha ujumbe maalum kwa walengwa ndani ya jamii liyopo kulingana na mazingira na maisha yao ya kila siku.

Pindi wanapokuwa vitani, safarini, jando, machungani au hata katika kupambana na wanyama wakali dhidi ya mifugo yao,hutumia nyimbo kama silaha pekee ya kujipa moyo wa ushujaa na ujasiri. Vilevile pia nyimbo hutumika katika matambiko, maombi na sherehe mbalimbali.

Japo kuwa kuimba na kucheza ni kawaida na ni utamaduni unaotambulika katika jamii ya wamaasai, lakini papo hapo kuna waimbaji waliobahatika kuwa na vipaji maalum ambao huchaguliwa na kuwa viongozi wa makundi ya kuimba kutokana na vipaji walivyonavyo.

Hivyo basi Yamat ni kati ya wale waliobahatika kuwa na kipaji hiki. Yamat alitambulika kuwa ana kipaji na uwezo mkubwa wa kucheza na kuimba tangu akiwa na umri mdogo sana. Na baada ya jando aliteuliwa na wanakijiji wa "ELUWAI" kuwa ni mwimbaji wa pili katika kijiji chao kutokana na rika lake.

Merege alikutana na Gsan mwaka 1999 alipokwenda kutembelea kijiji hicho, ndipo Gsan alipovutiwa na uimbaji wa Merege katika sherehe ya jando.Na hapo ikawa ndio mwanzo wa kujuana, kutembeleana, kuzungumza, kushauriana na kujadili ni jinsi gani mziki wa jamii yake unavyoweza kuuvutia Ulimwengu pale utakapochanganywa na vionjo vya miziki ya jamii nyingine za kimataifa.

Kwa maana hiyo ndipo walipokubaliana na kuamua kuchanganya na muziki wa "HIP HOP". Kwa sasa wamepata mafanikio makubwa ambapo walishapata mwaliko wa kufanya maonyesho ya muziki kwa ushirikiano wa "XPLASTAZ" pamoja na "FORTUNE TELLAZ"ambayo yalifanyika nchini Uholanzi chini ya udhamini wa "FESTIVAL MUNDIAL" mwezi wa sita mwaka 2001. Merege ameshiriki baadhi ya nyimbo kama DUNIA DUDUMIZI, AH-HAA na USHANTA ambazo zinapatikana katika album ya kundi la "XPLASTAZ" ijulikanayo kwa jina la ushanta.